Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, shirika rasmi la habari la Uturuki limeripoti kwamba; kundi la wadukuzi la Hanzala linalohusishwa na Iran, limechapisha taarifa binafsi za wanajeshi 69 wa Israel ambao inadaiwa walishiriki katika shambulio dhidi ya “Msafara wa Kimataifa wa Sumud”.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kundi la Hanzala lilichapisha katika akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa X taarifa zinazohusiana na wanajeshi wa kikosi cha majini cha Shayetet 13 cha jeshi la Israel. Katika taarifa yake, kundi hilo liliwataja wanajeshi wa Israel waliokuwa wamehusika katika shambulio dhidi ya msafara uliokuwa umebeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Ghaza kuwa ni “wachochezi wa machafuko baharini.”
Kundi hilo la wadukuzi pia lilitangaza kwamba; limeweka zawadi ya dola za Marekani 100,000 kwa kila mwanajeshi wa Israel ambaye taarifa zake zimechapishwa.
Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, kundi la Hanzala lilimuelekezea ujumbe Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa Israel, pamoja na wanachama wa baraza la mawaziri la utawala huo, likisema kwamba; wanachama wote wa serikali ya Israel wako chini ya “ufuatiliaji wa kidijitali na wa moja kwa moja.”
Hata hivyo, hadi sasa maafisa wa Israel hawajatoa tamko rasmi kuhusu usahihi wa taarifa zilizochapishwa.
Kundi hilo hapo awali pia lilidai kwamba; lilifanikiwa kupenya vifaa vya kielektroniki vya Herzi Halevi, mkuu wa zamani wa majeshi ya Israel, na kuchapisha picha pamoja na video zilizodaiwa kuwa za siri.
Aidha, Hanzala hapo awali lilitangaza kuwa; lilidukua simu za Naftali Bennett, aliyekuwa waziri mkuu wa Israel, Ayelet Shaked, aliyekuwa waziri wa sheria, pamoja na mshauri mkuu wa Benjamin Netanyahu.

Maoni yako